Friday, October 19, 2012

POLISI WAOMBA KUJIFUNZA ONLINE JOURNALISM



Katibu Rukwa Press Club Sammy Kisika akisalimiana na kamanda wa polisi mkoani Rukwa Jacob Mwaruanda ofisini kwake jana.





Kamanda wa jeshi la polisi akisalimiana na Mkufunzi wa habari wa mtandaoni Lukelo Mkami

Willy sumia
JESHI la polisi mkoani Rukwa limeutaka muungano wa vyama vya waandishi wa habari nchini UTPC kutoa mafunzo ya uandishi wa habari mtandani kwa maaskari wake ili waweze kuwa na mchango bora kwa waandishi wa habari kwa kutumia mitandao mkoani humo.
Akizungumza na mkufunzi wa tekinolojia ya habari za mtandaoni Lukelo Mkami alipofika ofisini kwa kamanda wa polisi mkoa humo Jacob Mwaluanda alisema kuwa mafunzo hayo yanarahisisha sana ufikishaji wa habari kwa wananchi kwa muda mfupi zaidi badala ya kutegemea vyombo vya habari vya kitaifa.
Mwaluanda alisema jana oktoba 18, 2012 kuwa katika mazingira ya kiutendaji kazi katika mkoa wake jeshi lake linategemea sana uungwaji mkono na ushuiriki mkubwa wa waandishi wa habari ili kufanikisha shughuli za jeshi la polisi kuwatumikia wananchi kwa ufanisi mkubwa zaidi na hivyo utaalamu waliopewa waandishi wa habari mkoani humo ni muhimu sasa UTPC kuangalia uwezekano wa kuwapa mafunzo kama hayo na vijana wake.
“Ukweli ni kuwa sisi jeshi la polisi tungependa pia mafunzo kama haya yatufikie na sisi ili tujue nini kinachoendelea pamoja na kuturahisishia kuwa na mawasiliano ya karibu na waandishi wa habari wetu wa mkoani Rukwa.” Alisema Mwaluanda
Akizungumzia maboresho ya kiutendaji kazi ndani ya ofisi yake kamanda wa polisi mkoani humo alisema ofisi yake inakusudia kubadili mfumo wa utoaji habari kwa waandishi wa habari Press Release kwa kuanza kutuma moja kwa moja katika mtandao kwa kutumia anwani za email ya mwandishi husika na hivyo itasaidia kupatikana habari za polisi kwa wakati na haimulazimishi mwandishi kuhudhuria kikao.
Mkufunzi wa mafunzo ya tekinolojia ya habari za mtandaoni, Lukelo Mkami alisema kuwa licha ya kujifunza tekinolojia waandishi wa habari pia wamefundishwa maadili ya uandishi wa habari zenye maadili katika mitandao yao maarufu kama blogs ili kutofautisha blogs za wataalamu na za wasio na utaalamu wa habari.
Alimsihi kamanda Mwaluanda kuwa na ukaribu na waandishi wa habari siyo kwa ajili ya habari pekee bali pia katika suala zima la elimu kwa umma juu ya suala la majukumu ya polisi kama vile polisi jamii, utii wa sheria bila shuruti na ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Katibu wa Rukwa Press Club, Sammy Kisika alisema umefika sasa wa jeshi la polisi na waandishi wa habari mkoani Rukwa na Katavi kubadili mwelekeo na kuanza ukurasa mpya wa kiutendaji kwa mshikamano zaidi ili kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi wa mikoa hiyo na kusahau yaliyopita.

AJALI KWA UZEMBE AU BAHATI MBAYA
UBEBAJI KAMA HUU NI HATARI
BODA BODA MTATUMALIZA WATEJA WENU
WANANCHI mkoani Katavi wanalalamikia madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda kwa kusababisha ajali za mara kwa mara kutokana na kitendo cha kutokuwa na ujuzi wa kutumia chombo hicho na kuwakimbia polisi wa usalama barabarani.
Kauli hiyo inafuatia taarifa iliyotolewa katika uzinduzi wa kamati mpya ya usalama barabarani ya mkoa wa Katavi, kaimu kamanda wa polisi Mrakibu Mwandamizi wa polisi Joseph Myovella alisema, ‘ukosefu wa elimu ya usalama barabarani ulichangia baadhi ya majeruhi kupata ulemavu wa kudumu na wengine kupoteza maisha’.
Watu 18 walikufa na wengine 215 kujeruhiwa katika jumla ya ajali 211 zilizotokea katika kipindi cha miezi minne toka  kuanzishwa kwa mkoa Mpya wa Katavi kuanzia Julai mwaka huu. Myovela alifafanua kwa kutaja takwimu.
Kati ya ajali hizo waendesha  pikipiki maarufu kwa jina la boda boda wanatuhumiwa kusababisha jumla ya ajali 96  ambazo zinadaiwa kutokea kutokana na uzembe wa kutojua sheria za usalama barabarani na kuwakimbia askari wanapotaka kuwapa ushauri.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt Rajabu Lutengwe na Mwenyekiti wa kamati hiyo Nassoro Arfi wakizungumza katika siku ya kuadhimisha siku ya usalama barabarani mwishoni mwa wiki  walilitaka jeshi la polisi kujipanga vizuri ili  kupunguza matukio ya ajali za barabrani zinazotokea mara kwa mara mkoani humo na kunusuru  maisha ya watu.
Baadhi ya madereva wa pikipiki mkoani humo ambao wamelipongeza jeshi la polisi kwa jitihada za kuhakikisha ajali za barabrani zinapungua kwa kutoa mafunzo, walisema kuwa kwa sasa wao watakuwa ni chachu ya kupunguza matukio ya ajali za barabarani na kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na hawatawakimbia tena kwani kifo hakichagui.



No comments:

Post a Comment